Skip to content
Gospo FM Radio 99.1 FM, Ishara ya Upendo

UPINZANI WAIKOSOA IEBC

26 Novemba 2026 · Kenya

Viongozi wa upinzani wameongeza shinikizo kwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka IEBC

Viongozi wa upinzani wameongeza shinikizo kwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka IEBC, wakitaka itoe mwelekeo wa haraka kuhusu usajili wa wapiga kura wapya kufuatia kumalizika kwa mkataba wake na kampuni ya Smartmatic International Holdings.

Wakizungumza katika mkutano na wanahabari jijini Nairobi, Novemba 25, 2026, viongozi hao wakiongozwa na aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua wamesema kukosekana kwa mfumo mpya wa usimamizi wa uchaguzi kunazua wasiwasi kuhusu maandalizi ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2027 pamoja na uchaguzi mdogo wa Mwingi Magharibi.

Gachagua amemtaka mwenyekiti wa IEBC Erastus Ethekon kutoa maelekezo kuhusu hatua zinazofuata, akitishia kuhamasisha Wakenya kuishinikiza tume hiyo ikiwa haitashughulikia malalamishi ya upinzani.

Kwa upande wake, aliyekuwa Jaji Mkuu David Maraga ameitaka IEBC kuweka vituo vya usajili wa wapiga kura katika maeneo mbalimbali nchini Marekani ili kurahisisha usajili wa Wakenya wanaoishi ughaibuni.

Aidha, Maraga amesema muungano wa upinzani umeandaa mswada unaolenga kurejesha kifungu cha 39 cha Sheria ya Uchaguzi kuhusu utangazaji na usambazaji wa matokeo ya uchaguzi, akisema hatua hiyo inalenga kuimarisha uwazi katika uchaguzi wa 2027