Skip to content
Gospo FM Radio 99.1 FM, Ishara ya Upendo

SERIKALI YATANGAZA HATUA ZA KUREJESHA AMANI

26 Novemba 2026

Serikali imetangaza mikakati mipya ya kuimarisha usalama na kurejesha amani katika maeneo ya mpakani mwa kaunti za Isiolo na Garissa kufuatia visa vya mapigano baina ya jamii vilivyosababisha vifo na uharibifu wa mali.

Serikali imetangaza mikakati mipya ya kuimarisha usalama na kurejesha amani katika maeneo ya mpakani mwa kaunti za Isiolo na Garissa kufuatia visa vya mapigano baina ya jamii vilivyosababisha vifo na uharibifu wa mali.

Hatua hizo zimeafikiwa katika kikao cha mashauriano kilichoongozwa Jumanne na Waziri wa Usalama wa Ndani, Kipchumba Murkomen, kilichowakutanisha viongozi kutoka kaunti hizo mbili kujadili hali ya usalama.

Miongoni mwa maazimio ni operesheni maalum inayoongozwa na taarifa za kiintelijensia, chini ya Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja, ya kukusanya silaha haramu katika maeneo hayo.

Kanja pia anatarajiwa kupitia upya usambazaji wa maafisa wa usalama, kuongeza vituo vya polisi na kuimarisha doria katika maeneo yaliyoathiriwa na machafuko.

Aidha, serikali itapitia utendakazi wa walinzi wa akiba wa polisi, NPR, kuwafanyia uhakiki na mafunzo upya, huku wale watakaobainika kutumia vibaya silaha zao wakibadilishwa.

Katika juhudi za kushughulikia chanzo cha migogoro, viongozi wamekubaliana kuimarisha kamati za amani, kuweka mfumo wa ugavi wa rasilimali baina ya jamii na kushirikiana na kampuni za mawasiliano kuboresha mtandao katika maeneo yaliyoathiriwa.

Hatua hizi zinajiri huku takriban watu 10 wakiuawa katika mapigano yaliyoshuhudiwa katika eneo hilo ndani ya wiki moja.