MIKAKATI YA LINDA MWANANCHI
26 Novemba 2026 · Kenya

Chama cha Equitable chataka kesi inayozuia mchakato wa kubadilisha utambulisho wa Linda Mwananchi itupiliwe mbali
Chama cha The Equitable Party (TEP) kimeliomba Baraza la Migogoro ya Vyama vya Siasa (PPDT) kutupilia mbali kesi inayolenga kuzuia mchakato wake wa kubadili jina na kuwa 'Linda Mwananchi Movement', kikisema kuwa mlalamikaji hana sifa za kisheria za kupinga uamuzi huo.
Katika hati ya kiapo ya kujibu madai iliyowasilishwa mbele ya Baraza hilo jijini Nairobi, Katibu Mkuu wa chama hicho, Italima Motanya, alieleza kuwa mlalamikaji, Emmanuel Willyngtone Khamala, alijiunga na chama hicho baada ya Kamati yake ya Kitaifa ya Utendaji (NEC) kuwa tayari imepitisha uamuzi wa kubadili jina.
Motanya alibainisha kuwa Khamala alijiunga na chama hicho mnamo Oktoba 11, 2026—siku tatu baada ya NEC kupitisha uamuzi huo mnamo Oktoba 8—jambo linalozua maswali kuhusu mazingira ya uanachama wake na hatua yake ya kufungua kesi hiyo.
"Muda ambao mlalamikaji alijiunga na chama, na hatua iliyofuata ya kuanzisha shauri hili, vinazua maswali ya msingi kuhusu nia yake," alisema Motanya.
Chama hicho pia kilihoji hali ya uanachama wa Khamala, kikidai kuwa hakuwasilisha cheti cha uanachama kama inavyotakiwa chini ya Ibara ya 5.1.6 ya Katiba ya chama hicho.
Aidha, Motanya alipinga mamlaka ya Baraza hilo kusikiliza shauri hilo, akidai kuwa Khamala alishindwa kutumia kikamilifu taratibu za ndani za chama za kutatua migogoro, kama ilivyoelekezwa katika Kifungu cha 40(2) cha Sheria ya Vyama vya Siasa.
